Mashindano ya shule za upili hatua ya kaunti ya kilifi kwenye muhula huu wa pili yalianza kwa kasi hapo jana siku ya kwanza katika eneo bunge la Malindi.
Takriban wanafunzi 1500 waliwasili katika mji wa Malindi na wanashiriki katika mashindano hayo. Mcdonald Mzungu Udzile, ambaye ni katibu wa michezo ya shule za upili za Kilifi amefafanua kuwa mashindano haya yalikuwa yanafaa yafanyike katika eneo bunge la Kaloleni lakini shule ambazo zingekuwa wenyeji wa mashindano hayo St Georges na St Johns hazikuwa na utayari.
”Mashindano haya yalikuwa yafanyike katika eneo bunge la Kaloleni lakini kulitokea matatizo kwenye mazungumzo na washikadau na ikabainika kuwa hawatakuwa na uwezo wa kuwa wenyeji. Yalikuwa yafanyike St Georges na St John lakini hilo halikuwezekana.” Alisema Udzile
Udzile anasema ana matumaini makubwa kuwa mwaka huu watapata vikosi bora vya kushindana katika ngazi ya mkoa wa Pwani mashindano yatakayofanyika katika shule ya upili ya Oda kaunti ya Tana River na baadaye kuelekea katika kaunti ya Kisii ambako ngazi ya kitaifa itafanyika.
”Raundi hii kwa ubora uliopo viwanjani, nina imani kuwa tutapata timu nzuri zitakazotuwakilisha katika mashindano ya kimkoa kuelekea Oda, Tana River mwaka huu.” Aliongeza Udzile.

