MACHUNGAJI LEONARD KOTSE ATOA WITO KWA MUUNGANO WA KENYA KWANZA KUSITISHA MAANDAMANO

Mchungaji wa kanisa la Adonai kaunti ya Mombasa Leonard Kotse, ametoa wito kwa viongozi wa azimio kusitisha maandamano yao na badala yake watafute njia mbadala ya kuiwajibisha serikali.
Katika mazungumzo ya kipekee na Meza yetu ya habari kwa njia ya Simu, Mchungaji Kotse amesema ni vyema iwapo maandamano hayo, yatasitishwa na mikakati kuwekwa namna masuala mbalimbali yatatatuliwa bila kuonyeshana ubabe wa kimirengo.
Akinukuliwa wakati wa kutayarishwa kwa taarifa hii, mchungaji Kotse ametilia shaka swala kuwa maandamano hayo yatakuwa ya amani akisema kuwa mara nyingi kwenye historia ya taifa la Kenya kunashuhudiwa uharibifu mwingi wa mali sawia na umwagikaji wa damu kunapoandaliwa maandamano.
Aidha, amewataka Wakenya kusimama kwenye zamu na kuliombea taifa la Kenya, ili liepukane na baadhi ya changamoto ambazo huenda zikalemaza nchi kimaendeleo.