Mchezaji wa zamani wa klabu ya Barcelona Andres Iniesta, ambaye ni mshindi mara mbili wa kombe la Euro na Kombe la Dunia la 2010 akiwa na timu ya taifa ya Uhispania, ametangaza kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 40 hii leo.
Iniesta alijulikana katika ulimwengu wa soka kupitia akademia maarufu ya La Masia ya Barcelona na alijipatia nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza timu mwaka 2002 akiwa na umri wa miaka 18 tu, na kuwa nguzo kuu katika kiungo kabla ya kuondoka kwake miaka 16 baadaye.
Alishinda mataji tisa ya La Liga na Ligi ya UEFA mara nne akiwa na Barcelona, lakini wakati wake mkubwa ulikuja katika fainali ya Kombe la Dunia ya 2010 wakati alifunga bao la ushindi dhidi ya Uholanzi.
Baada ya kuondoka Barcelona mwaka 2018, Iniesta alitumia miaka mitano na klabu ya Japan Vissel Kobe kabla ya kucheza msimu mmoja wa mwisho katika milki za kiarabu.
Leo ndio tarehe 8 na ametoa tangazo hilo kutokana na kuenzi nambari nane (8) ambayo ni nambari ya jezi aliyoienzi miaka mingi yake ya soka la kulipwa.

