Wajumbe kutoka mataifa ya Afrika Mashariki pamoja na Ethiopia wamekongama Mombasa kwa warsha ya kujadili uundaji sera zinazolenga kuleta usawa wa kijinsia miongoni mwa wasichana na wanawake.
Warsha hiyo ya siku mbili inajumuisha mashirika ya kutetea haki za wanawake na kukomesha dhuluma dhidi ya wasichana.
Mjumbe wa bunge la kaunti ya Mombasa Milcah Moraa Ngare muasisi wa mpango wa SHE LEADS amesema katika kongamano hilo wanalenga kuangazia changamoto zinazowakumba wasichana na jinsi zinavyoweza kutatuliwa.
Moraa amesema kuwa wajumbe wa kike kaunti hiyo pia wamejitwika jukumu la kuhakikisha kuwa wanaidhinisha miswada inayotetea haki za watoto wa kike huku akisema hali ya umaskini imechangia kwa wasichana wengi kuingia katika ndoa za utotoni.
Aidha amefichua kuwa kwa sasa tayari wamebuni sheria mpya ambazo zitatumika kutetea haki za watoto sawia na kuwalinda watoto wa kike dhidi ya dhulma za kijinsia.
KONGAMANO LA KUJADILI UUNDAJI SERA ZINAZOLENGA KULETA USAWA WA KIJINSIA UNAENDELEA MOMBASA

