BILLY Munyiri Mwangi, mwanafunzi wa chuo aliyetoweka baada ya kutekwa nyara na wanaume wanne waliovalia barakoa katika mji wa Embu, amepatikana akiwa hai.
Kulingana na familia yake, Mwangi, ambaye alionekana kuwa dhaifu, alifika nyumbani Jumatatu asubuhi na kupelekwa hospitalini, kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 24, alitekwa na watu ambao bado hawajajulikana hadi sasa, alipokuwa akisubiri kuhudumiwa kwenye kinyozi katika mji wa Embu tarehe 21 Jumamosi Desemba mwaka 2025.
Babake kijana huyo kwa jina Gerald Karicha, mnamo Januari 2 mwaka huu wa 2025, aliambia Mahakama Kuu jijini Nairobi kwamba, watekaji nyara wa Mwangi walikuwa wamemfuata kwa siku kadhaa, kabla ya kumchukua kwa nguvu.
Karicha alimwambia Jaji Bahati Mwamuye, kuwa gari lililo tumika kutekeleza uovu huo lilikuwa aina pick up Double Cabin, huku lililokuwa likimfuata likiwa aina ya Toyota Fielder la rangi nyeupe, nambari za usajili KDG 527 D.

