Timu ya taifa ya Kenya Shujaa sasa imeshushwa daraja kutoka kwa mashindano ya raga ya World Sevens Rugby Series baada ya kutandikwa kichapo kichungu cha alama 12-7 dhidi ya Canada.
Kushuka huko sasa kunamaanisha kwamba Kenya haitashiriki katika mashindano ya HSBC ya mwaka 2024 na huenda pia ikashindwa kufuzu kwa mashindano ya olympiki ya Paris Ufaransa. Kwa sasa Kenya Shujaa italazimika kutandikana vikali na wababe wa hapa Afrika akiwemo Afrika Kusini ambao ni vigogo wa raga za dunia katika kupigania nafasi yao ya kuingia katika mashindano ya olimpiki.
Hii ni mara ya kwanza baada ya miaka 20 Shujaa inashuka daraja katika raga za dunia. Kwa muda sasa timu za raga za taifa hili zimekuwa zikiyumba kikubwa kikitajwa kuwa uongozi mbaya katika ngazi za kitaifa.
Matukio hayo yamezidi kuzua hisia mbalimbali miongoni mwa mashabiki wa raga hapa nchini wengi wao wakishinikiza kuwepo kwa marekebisho katika uongozi wa kitaifa wa raga ili kukomboa mchezo huo ambao ni kati ya michezo iliyowahi kuweka Kenya katika rada za dunia katika miaka ilopita.

