Naibu kamishna kaunti wa Tana river, John Kipsiwa amewashinikiza wanajamii Tana delta kubuni sera za maelewano baina yao kwa minajili ya kudhibiti mizozo kati yao hasa wakulima na wafugaji.
Akizungumza katika mkutano uliowaleta viongozi wa serikali kuu, serikali ya kaunti na mashirika mbalimbali, Kipsiwa amesema mizozo ya mara kwa mara baina ya wafugaji na wakulima huchochea utovu wa usalama.
Aidha Kipsiwa amewataka wakaazi kutojihusisha na maswala ya kisiasa ikizingatiwa kwamba wakati wa siasa umeisha na badala yake akasisitiza haja ya uwiano na utangamano miongoni mwao.
Wakati uo huo mwanaharakati wa masuala ya amani, Hassan Moroa amekariri kuwa kuna haja ya kuwekwa kwa mikakati ya kutatua mizozo baina ya wafugaji na wakulima ikiwemo kutoa hamasa za mara kwa mara kwa jamii hizo kuhusiana na umuhimu wa amani.

