Mwenyekiti wa shirika la usalama Tana River peace reconciliation and development, (TRPRD) kaunti ya Tana River Harrison Moroa amesema hali ya kiangazi katika kaunti ya Tana River ni ya kutiliwa hofu mno.
Akizungumuza katika kikao cha kutathmini athari ya hali ya kiangazi eneo la Tana Delta, Moroa amewataka wakazi wa Tana River kudumisha amani wakati huu wa kiangazi.
Moroa amesema ukosefu wa chakula na uhaba wa maji umezidi kuwaathiri wakazi wa kaunti ya Tana River na kuyaomba mashirika na serikali kutoa msaada ili kukabiliana na hali hiyo.
Wakati uo huo amezitaka kamati za usalama na kamati za raslimali eneo la Tana Delta kushirikiana ili kupunguza uwezekano wa ukosefu wa usalama eneo la Tana Delta ambako idadi ya wafugaji wa kuhama hama wameongezeka maradufu.
Aidha, amedokeza kuwa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano wameathirika na utapiamlo katika kaunti hiyo na kuisihi serikali ya kaunti na mashirika kutoa msaada wa chakula kwa jamii wanaokumbwa na baa la njaa kutokana na hali ya ukame kuendelea kukithiri katika kaunti hiyo.

