HISIA MBALIMBALI ZAENDELEA KUTOLEWA NA VIONGOZI WA KIDINI MJINI MALINDI KUHUSU MAANDAMANO

Baadhi ya viongozi wa kidini mjini Malindi kaunti ya Kilifi wamepinga maandamano ambayo muungano wa Azimio la Umoja One Kenya unapania kuandaa siku ya Jumatatu wiki ijayo, ili kupinga uongozi wa rais William Samoei Ruto.
Wakiongozwa na Askofu wa kanisa la JCC Malindi kaunti ya Kilifi Thomas Tsuma Kakhala, ametoa wito kwa viongozi hao kutafuta mbinu mbadala za kusuluhisha tofauti zilizoko kati yao, pasi na kuathiri amani na uchumi wa taifa hili.
Akizungumza na wanahabari nje ya majengo ya kanisa hilo mjini Malindi, Askofu Kakhala amesema wapo viongozi wakuu na walio na elimu ya juu, katika mirengo yote miwili ambao wanaweza kuwaleta pamoja viongozi hao kuandaa mazungumzo ambayo, yatachangia kuwaunganisha Wakenya na sio kuwagawanya.
Kwa upande wake mchungani wa kanisa la Christ The King Baptist mjini Malindi kaunti ya Kilifi, Francis Katana ameunga mkono kauli hiyo huku akisema licha ya katiba kuwapa wakenya Uhuru wa kushiriki maandamano, taifa hili halijaweza kutekeleza maandamano ya amani na hivyo basi huenda sekta ya utalii eneo la Pwani ikaathirika iwapo maandamano hayo yataandaliwa.