GAVANA ANDREW MWADIME AWEKA MIKAKATI KUWAKABILI WAFANYIKAZI HEWA TAITA TAVETA

Serikali ya kaunti ya Taita Taveta inaendelea kufanya ukaguzi kwa madereva wanaofanya kazi katika kaunti hiyo kwa minajili ya kujua idadi yao kamili jambo litakalowezesha serikali hiyo kuwatambua wafanyikazi hewa.
Akizungumza kabla ya kuanzishwa kwa ukaguzi huo ambao haukufanyika tu kwa madereva lakini pia idadi kamili ya magari yanayomilikiwa na kaunti, gavana wa Taita Taveta Andrew Mwadime amesema kuwa analenga kupunguza mzigo wa mishahara kwa asilimia 35.
Mwadime amesema kuwa ni sharti madereva hao wawajibishwe huku akiahidi kuwa kila sekta kwenye kaunti hiyo itafanyiwa ukaguzi kubaini wafanyikazi hewa.
Gavana Mwadime amesema kuwa wafanyikazi hewa ndio chanzo cha kurejesha maendeleo nyuma ikizingatiwa kwamba wanapokea mishahara ilhali hawafanyi kazi yoyote kwenye kaunti hiyo.