Serikali ya kaunti ya Kilifi itaendelea kushirikiana na serikali ya kitaifa ili kuinua sekta ya uvuvi na uchumi wa raslimali za baharini kwa kuanzisha na kuendeleza miradi itakayosaidia kuboresha maisha ya wakaazi.
Haya ni kulingana na Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro ambaye amesema kuwa ujenzi wa makao makuu ya sekta hizo utafanyika katika eneo la Old Ferry mjini Kilifi.
Aidha amethibitisha kuwa tayari kuna baadhi ya miradi ya ujenzi wa masoko ya kisasa ya wavuvi inayoendelezwa na serikali ya kaunti , miradi hiyo ikitarajiwa kukamilika hivi karibuni kabla ya uzinduzi rasmi.
Kwa upande wake, katibu katika wizara ya madini na maswala ya uchumi wa raslimali za baharini Nchini Betsy Njagi amesema serikali ya kitaifa ikishirikiana na benki kuu ya dunia itazindua miradi tofauti tofauti katika kitengo cha ubaharia eneo la Pwani.
Njagi amesema hivi karibuni watatangaza zabuni kuhusu miradi hiyo ili kazi zianze rasmi, lengo kuu likiwa ni kuboresha uchumi wa raslimali za baharini kaunti ya Kilifi na Pwani kwa jumla.

