Kocha wa timu ya taifa Harambee stars Engin Firat amesema bado kuna matumaini ya Kenya kufuzu kwa AFCON 2025 licha ya matokeo ya kutoridhisha ya sare tasa katika mechi ya kwanza dhidi ya Zimbabwe.
USIKU wa leo mwendo wa saa moja Harambe stars watakuwa wanashuka dimbani tena kwa mechi ya pili dhidi ya Namibia katika taifa la Africa kusini kutokana na Namibia kukosa kuwa na kiwanja cha hadhi ya kimataifa kwa mujibu wa Caf na shirikisho la soka la Dunia Fifa.
Ni tatizo ambalo pia lipo Kenya kwani harambee Stars ililazimika kucheza mechi yake ya nyumbani wiki jana Uganda.
Kocha huyo anaelekea kwenye mechi ya leo na shinikizo kutoka kwa mashabiki wa kenya ambao wanadai matokeo bora kutoka kwake na angalau kuipa fahari Kenya.
Hata hivyo kocha huyo yupo na changamoto ya majeruhi katika kikosi chake baada ya Michael Olunga kuthibitika kuwa atakosekana kwenye mechi hiyo baada ya kupata majeraha katika klabu yake ya Al Duhail.

