BUNGE LA KAUNTI YA KWALE LAPITISHA BAJETI YA ZIADA YA SHILINGI MILIONI 25

Bunge la kaunti ya Kwale limepitisha bajeti ya ziada ya shilingi milioni 25, zitakazotumika kuboresha huduma katika hospitali ya rufaa ya Msambweni.
Mwakilishi wa wadi ya Ramisi kaunti ya Kwale, Hanifah Mwajirani amesema fedha hizo zinalenga kuimarisha shughuli za utoaji matibabu katika hospitali hiyo.
Mwajirani ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti ya Kwale, amesema hatua hiyo itawawezesha wakaazi kupata huduma bora za afya.
Wakati huohuo, ameeleza kuwa fedha hizo pia zitatumika kuwaajiri mabawabu ili kuimarisha usalama katika hospitali hiyo na watashirikiana na askari wa kaunti ya Kwale, ili kukabiliana na visa vya wizi vilivyokithiri katika hospitali hiyo ya rufaa ya Msambweni.