Idadi kubwa ya wanajamii katika wadi ya Shella mjini Malindi kaunti ya Kilifi wamenyooshewa kidole cha lawama kwa kususia kikao cha wananchi kutoa maoni yao, kuhusiana muongozo wa utendakazi wa serikali ya kaunti ya Kilifi katika hatamu yake ya uongozi wa miaka mitano.
Kwa mujibu wa msimamizi wadi hiyo ya Shella Zamzam Mohammed, huenda matakwa ya wananchi katika wadi hiyo sasa yakakosa kujumuishwa katika mipangilio ya serikali ya Kaunti ya Kilifi, kutokana na hatua ya wao kukosa kuhudhuria kikao hicho.
Katika mahojiano ya kipekee na mwanahabari wetu kwenye ukumbi wa Manisapa mjini Malindi kaunti ya Kilifi, ameeleza kuwa huenda kukashuhudiwa changamoto kuu katika utekelezaji wa matakwa ya wananchi wa eneo hilo, hasa yale ambayo yamekosa kujumuishwa katika nakala rasmi ya mapendekezo hayo kwa serikali ya kaunti ya Kilifi.
Kauli hiyo imeungwa mkono na msimamzi mkuu wa shirika la kutetea haki za kibinadamu la Haki Yetu kaunti ya KIlifi, Warda Zighe ambaye ameeleza kuwa licha ya viongozi wa kijamii pamoja na wale wa mashirika ya kijamii kujitokeza katika zoezi hilo, huenda baadhi ya matakwa ya wananchi wa wadi ya Shella yakakosa kutekelezwa na serikali ya kaunti ya Kilifi.
IDADI NDOGO YA WENYEJI WA SHELLA KAUNTI YA KILIFI YAJITOKEZA KWENYE KIKAO CHA WANANCHI KUTOA MAONI

