Huenda klabu ya Young Bulls Starlets kutoka Malindi kaunti ya Kilifi ikaingia kwenye ligi za FKF kwa mara ya kwanza kabisa msimu ujao baada ya timu hiyo kubuniwa mwaka huu 2024.
Rishadi Shedu, mkufunzi anayesimamia kikosi hicho amethibitisha kuwa msimu huu walikosa nafasi kutokana na kuchelewa kusajiliwa lakini walihusika pakubwa katika mashindano ya Chapa dimba na Safaricom ambayo yalifanyika katika kaunti ya Mombasa kwenye mkoa huu wa Pwani.
Amethibitisha kuwa Malindi kuna talanta nyingi za kinadada lakini wamekosa kushikwa mkono na huenda wakapotea iwapo hawatashikwa mkono, hilo ndio jambo kuu lililowalazimu kuzindua timu hii yakinadada.
Amesema kuwa ukanda huu wa pwani kuna wachezaji wa kike wanaofanya vyema kimataifa jambo ambalo anahisi linaweza kuchochea wengi zaidi wa kike kujituma ili kupata mafanikio viwanjani. Ameeleza pia imani yake kuwa Young Bulls Starlets itapanda madaraja hadi ligi kuu ya kinadada.
Ikumbukwe kwamba mwaka 2021 shirikisho la CAF lilitangaza sheria ya vilabu ambayo vitacheza mashindanio ya CAF kimataifa ni sharti wawe na timu za kinadada, na Young Bulls na Bulls Starlets ziko katika njia sawa kwa mujibu wa sheria hiyo ambayo imeanza rasmi kufanya kazi msimu huu 2023/2024.

