Klabu ya Mombasa All Stars huenda isiendelee kushiriki katika ligi ya fkf katika daraja la pili kutokana na mabosi wa timu hiyo kuondoa udhamini wao.
Hii ni kutokana na taarifa ambazo zimethibitishwa na baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo wanaodai kuwa huenda nafasi ya klabu hiyo ikauzwa kwa klabu ya Wananyuki baada ya mdhamini mkubwa wa timu hiyo kusafiri nje ya nchi kwa kile alichodai kuwa ni masuala ya kimatibabu katika taifa la India.
Taarifa zaidi zasema kuwa wachezaji hawakushiriki mechi dhidi ya Ziwani Youth kutokana na baadhi ya wachezaji hao kuisusia baada ya taarifa hizo kusambaa wiki jana.
Kulingana na baadhi ya wachezaji ni kuwa kwa sasa wachezaji wa Mombasa All Stars hawana timu kutokana na wananyuki kuibua taarifa kuwa klabu hiyo tayari inakuja na wachezaji wake, Hata hivyo mabosi wa klabu ya Mombasa All Stars wanasema wako tayari kuachilia wachezaji ambao watapata vilabu kutoka kwa orodha yao ya FKF–FIFA Connect.
Kabla ya klabu hiyo kusambaratika ilikuwa imesajili alama tatu pekee msimu huu baada ya mechi tatu.

