Mashindano ya shule za upili ya muhula huu wa pili katika kaunti ya Mombasa yameahirishwa hadi mwezi ujao baada ya kucheleweshwa kwa mgao wa Fedha wa kuandaa mashindano hayo.
Kulingana na katibu wa kamati andalizi ya michezo ya shule za upili kaunti ya Mombasa Silas Atsulu, michuano hii ilikuwa iandaliwe katika eneo la Jomvu na Changamwe lakini ikasitishwa baada ya ripoti ya kucheleweshwa kwa fedha kuwafikia.
Viongozi wa mashindano hayo wamezitaka timu kutumia muda huu kuendelea kujitayarishia michuano hii. Fainali hizi sasa zitaandaliwa kutoka tarehe 2 hadi tarehe 4 mwezi wa Julai.
Kaunti ya Kilifi pamoja na Tana River pia ni kati ya kaunti ambazo zimeahirisha mashidnano hayo kutokana na ukosefu wa fedha.

