MICHEZO YALETA WATU PAMOJA KILIFI

Idara tofauti za serikali kutoka kaunti ya Kilifi zimejumuika na wakaazi kwa lengo la kutangamana na kujenga uwiano.

Michezo mbalimbali imeandaliwa katika Chuo kikuu cha pwani huko Kilifi kuwaleta pamoja maafisa kutoka idara ya mahakama, polisi na idara ya mashtaka, wanabodaboda pamoja na wakaazi ili kuwahamasisha kuhusu ubora na kuelewa jinsi ya idara za serikali zinavyofanya kazi.

Fatuma Dulo komanda wa polisi kutoka kaunti ya Kilifi alikuwepo katika mashindano hayo na anasema yanalenga kusaidia jamii na idara mbalimbali za serikali kuwa kitu kimoja

”Tumeamua kuja na mpango huu ili kuleta watu wengi pamoja na idara tofauti za serikali ili kuleta utangamano na kusaidia wanajamii kutangamana. Sio lazima tukutane na raia wakati watu wamefanya makosa pekee.” Alisema bi Fatuma

Afisa wa Michezo kaunti ya Kilifi Naftali Owino anasema michezo ndio silaha kubwa zaidi ya kuleta watu pamoja katika jamii.

.”Leo hapa kumejaa watu pomoni kwa ajili ya kichezo na idara mbalimbali zipo hapa. Michezo ndio kifaa pekee unaweza kukitumia kupatanisha watu” Alisema Owino