Mashindano ya kitaifa ya KYISA yanaingia siku yake ya tatu leo katika kaunti ya Kilifi na takriban kaunti 20 za taifa hili zipo katika kaunti hii ya Pwani kwa ajili ya kupambania ubingwa wa makala hii ya tisa.
Michezo ya soka, basketball na voliboli ndio michezo inayoshirikishwa msimu huu. Huku ikiwa msimu huu ni msimu wa mvua michezo kadhaa inapitia changamoto ya kuchezeka.
Msimamizi na mkufunzi wa mpira wa vikapu katika kaunti ya Kilifi Frank Osogo analalamikia kucheleweshwa kwa ujenzi wa kiwanja cha kisasa cha mchezo huo kwani ratiba za jana zililazimika kuchelewa kuanza timu zikisubiri mvua kubwa kupusa kabla ya mechi kuanza.
”Tumekuwa tukilia na serikali kwa muda sasa angalau watujengee uwanja wa kisasa wa mchezo huu wa mpira wa vikapu lakini mambo bado yamesimama. Hatutachoka kuomba. Tutasubiri tulakini kwa sasa hali si nzuri kwa kweli.” Alisema Osogo.
Amesema kuna hatari ya wachezaji kuumia kutokana na utelezi ya viwanja vilivyopo hasa jinsi ambavyo kunaendelea kunyesha katika kaunti hii.

