Alex Shikangwa ambaye ni mkufunzi mkuu wa klabu ya Bandari Youth ambao ni mabingwa wa mashindano ya Chapa Dimba katika mkoa huu wa pwani kwenye makala yaliyopita amemmiminia sifa mwandishi wa habari za michezo na mpiga picha maarufu katika kaunti ya Kilifi Kaka Jabali kuwa mdau anaysaidia vijana wengi katika gatuzi hilo sio tu katika soka lakini pia katika masuala muhimu ya kijamii.
Amesema Jabali amekuwa akisaidia pakubwa kwenye suala la kusaidia timu kusaka talanta za wachezaji mashinani lakini pia kusaidia kurejelea masomo vijana ambao vijana ambao walikuwa wameacha kusoma.
”Kaka Jabali amesaidia vijana wengi sana huko Kilifi. Kuna vijana walikuwa wameacha shule na ni wachezaji, (Jabali) amewasaidia kwa kuwatafutia mashule sana. Ni mtu ambaye kama wakufunzi tuko na ukaribu sana naye kwani anatusaidia kusaka talanta za wachezaji. Tukihitaji mchezaji huwa tunawasiliana na kufanikisha jambo hilo.
Hata hili dili la Kavoi (lililotibuka dakika za mwisho) alihusika pakubwa manake tulimwona kwenye mashindano ya Chapa Dimba (Mombasa) tukavutiwa naye na baadae sasa ndio tukawasiliana na Jabali ndio sasa Kavoi akaja kwenye majaribio” Alieleza Shikangwa.
Kuhusu suala la Rafiki Kavoi ambaye wanalenga kumsajilikutoka klabu ya daraja la pili Malindi Progressive Academy mwisho wa msimu ni kuwa wanamchukua na kumrudisha shuleni kama Bandari kwa sasa lakini iwapo atahitajika kurudi Malindi Progressive Academy watamwachilia kwa sasa lakini kumsajili kama mchezaji huru mwisho wa msimu.
”Kwa sasa Kavoi tumemchukua tumsomeshe, atasoma huku Mombasa lakini iwapo watamhitaji (Malindi Progressive Academy) katika mechi zao basi wamchukue, lakini kwa sasa bila shaka lolote tutamsomesha Kavoi. Suala la kumsajili labda mpaka mwisho wa msimu kama mchezaji huru.” Aliongeza Shikangwa.
Katika mahojiano na Tama La Spoti kupitia njia ya simu, Kaka Jabali alidokeza kuwa kwa sasa hajakuwa wakala rasmi wa wachezaji lakini amezamia kozi ya uwakala na katika siku zijazo analenga kuwa wakala wa wachezaji.
Hiyo ni baada ya uvumi kuibuka miongoni mwa wadau mbalimbali wa soka kuwa Jabali anajihusisha na uwakala taaluma ambayo hajulikani nayo mashinani hasa vilabu vya Malindi majuzi vilitoa wasiwasi huo.

