SOKA LA ELIMU LARINDHIMA TEZO

Timu ya walimu wa shule za upili kutoka eneo la Chonyi kaunti ya Kilifi imewarambisha sakafu kwenye mchezo wa kirafiki uliojaa mbwe mbwe na mahanjam ya kila aina mjini Tezo.

Ngarambe hiyo iliyohusisha timu ya kabumbu ya walimu wa shule za upili kutoka eneo la Chonyi maarufu kikosi kazi imeonyesha umahiri ugenini kwa kupata ushindi wa mabao 3-2.

Kulingana na nahodha wa kikosi kazi Rodgers Ondiek, walimu wenzake wameamua kuungana na kusakata kabumbu kama njia ya kutafuta suluhu ya changamoto ya kuandikishwa kwa matokeo duni katika mitihani ya kitaifa kaunti ya Kilifi.

Kwa upande wake Mike Baya nahodha wa Tezo Veterans ameeleza kufurahishwa na hali ya mchezo huku akiwapongeza wapinzani wao kwa kuonyesha ubabe kwenye ngarambe hiyo.