DILI LA KAVOI LATIBUKA, ATASUBIRI MWISHO WA MSIMU

Dili la uhamisho linalohusisha Rafiki Kavoi mchezaji ambaye kwa sasa ni mali ya Malindi Progressive Academy kuelekea klabu ya Bandari Youth katika kaunti ya Mombasa litalazimika kusubiri hadi mwisho wa msimu pale ambapo mchezaji huyo ataweza kuhama kama mchezaji huyu baada ya jaribio la sasa kugonga mwaka kwa kile kinachotajwa kuwa uongozi wa klabu hiyo inayomilikiwa na mwakilishi wadi wa mji wa Malindi kaunti ya kilifi kugoma kumwachilia.

Alex Shikhanga ambaye ni mkufunzi wa klabu ya Bandari Youth akizungumza na Tama La Spoti hii leo amethibitisha kuwa walitambua talanta ya Kavoi kupitia mashindano ya Chapa dimba katika mkoa wa pwani yaliyofanyika katika kaunti ya Mombasa.

”Tulimwona Kavoi katika mashindano ya Chapa Dimba Mombasa na tukavutiwa naye, habari zaidi Kaka Jabali alitujuza kwamba ni kijana mwenye uwezo. Baadaye tumwalika kambini kwetu kwa majaribio na alionyesha kiwango kizuri na hapo ndipo tukaanza mchakato mzima wa kutaka kumsajili.” Alieleza Alex.

Kulingana na Alex ni kuwa Bandari Youth iliwasiliana na uongozi wa klabu ya Malindi Progressive Academy kupitia katibu mkuu Alex Jumba lakini wazo la kusajiliwa kwa Kavoi katika dirisha la sasa lilizidi kukosa kuzaa matunda kwani lengo la Bandari Youth ni kumrudisha mchezaji shuleni pamoja na kuichezea Bandari Youth. Hata hivyo Alex anasema Kavoi sasa atalazimika kufanya mazoezi bila kucheza hadi mwisho wa msimu huku akirejea masomoni.

”Kwa sasa kijana anarejea masomoni ila tunapania kuwasilisha rasmi ombi la kutaka kumsajili mwisho wa msimu kama mchezaji huru. Iwapo Malindi Progressive Academy watamhitaji kwenye mechi zao sisi hatuwazuii kwa lolote. Wamchukue (ni wao kwa sasa)” Aliongeza Alex.

Alex Jumba ambaye ni katibu mkuu wa klabu ya Malindi Progressive ameweka wazi kuwa watamwachilia Kavoi mwisho wa msimu ila kwa sasa wamemruhusu aendelee na masomo ya sekondari katika kaunti ya Mombasa.

”Kavoi kwa sasa ni mchezaji wetu kihalali na yuko katika ‘Systems’ zetu za FIFA Connect. Lakini hatumzuii asipate masomo kwa maana ni haki yake. Swala la kumwachilia labda mwisho wa msimu. Siwezi mpa mchezaji (Release) bila idhini ya kiongozi wetu Mh Rashid Odhiambo.” Alisema Jumba kupitia njia ya simu akizungumza na Tama La Spoti.

Kupitia mazungumzo ya simu mkufunzi wa klabu ya Malindi Clusters klabu iliyomzaa Kavoi, Coach Davis Badili ameibua tetesi kuwa huenda klabu ya Malindi Progressive kuna tatizo la wachezaji kuachiliwa wakati wanapotaka kuhama.

”Ni kama hapo MPA hilo suala la wachezaji kunyimwa ‘Release’ halijaanza sasa. Nasikitika na jinsi wanavyomfanyia mchezaji wangu wa zamani Kavoi. Kwa kweli nahisi kudharaulika na kukosewa heshima na jinsi Mh Rashid Odhiambo anavyotufanyia kwenye suala hili.” Alisikitika Badili.

Hii ni baada ya Badili na Kavoi kukutana na mheshimiwa Odhiambo  wikendi ilopita (Jumapili) kwa mazungumzo kuhusu uhamisho huo lakini hayakufua dafu. Vilevile Badili amethibitisha kuwa alikutana na Alex (Katibu mkuu wa MPA) lakini bado mazungumzo hayakufua dafu, Alex akisema kwamba hawezi achilia mchezaji bila idhini ya mheshimiwa.

Kwa sasa Kavoi hashiriki katika mashindano yoyote ya soka kutokana na suala hilo ila taarifa zasema kwamba amekuwa akijihusisha na mazoezi katika klabu ya Bandari Youth katika kaunti ya Mombasa.