Fainali za kombe la Chapa Dimba na Safaricom zilichezwa jana katika kaunti ya Mombasa kwenye uwanja wa KPA Mbaraki na ni mashindano ambayo yalishuhudia Changamwe Ladies wakichukua ubingwa wa fainali hizo kwa upande wa kinadada baada ya kuwalaza Bulls Starlets kutoka kaunti ya Kilifi kichapo cha mabao 3-0.
Kwa upande wa wanaume ni kuwa Bandari Youth iliibuka mabingwa wa mkoa wa pwani kwa kuwachapa the Young Gunners kutoka kaunti ya Tana River kichapo cha mabao 3-0.
Alex Shikanga ambaye ni kocha wa klabu ya Bandari Youth anasema kwamba wamekuwa na safari ndefu kulea vipaji kabla ya kujipata katika fainali na hatimaye kushinda ubingwa wa chapa dimba pwani.
Kwa wake Bernard Owour ambaye ni kocha wa Changamwe Ladies amehakikishia mashabiki wa klabu hiyo na pwani kwa jumla watajizatiti katika mashindano ya kitaifa mwaka huu akikiri kuwa yupo tayari kukabiliana na ushindani katika kiwango hicho.
Twahiri Muhidin ambaye ni mkurugenzi wa kiufundi katika klabu ya Bandari amethibitisha kuwa Pwani iko na vipaji na katika klabu ya Bandari tayari kupitia mashindano haya wamechukua wachezaji wawili.
Gloria Mupa kutoka Bulls Starlets ndiye aliibuka mfungaji bora wa mashindano hayo kwa upande wa kinadada baada ya kucheka na wavu mara tano.
Hamisi Nyale straika wa klabu ya Bandari Youth aliibuka mchezaji bora mwenye thamani zaidi maarufu kama MVP.

