Mkufunzi wa klabu ya Malindi Progressive Academy Nero Chishenga amesema kuwa yuko na imani kubwa atasajili ushindi dhidi ya klabu ya Inter Dabaso watakapovaana wikendi hii katika mechi ya ligi ya daraja la pili kitaifa.
Kulingana na Nero ni kuwa kikosi hicho kwa sasa kimeanza kushika kasi tofauti na kinayodhaniwa kuwa hafifu na ametuma onyo kwa Inter Dabaso akisema kwamba wanajiimarisha vilivyo kwa ajili ya mchuano huo.
Mkufunzi huyo aidha anasema kuwa bado ana matumaini ya kumaliza katika nafasi nzuri licha ya mwanzo mbovu msimu huu na kwa uzoefu wake katika ligi hii na anasema bado anasuka kikosi chake na mbele kuna mwangaza tofauti na mwanzo usioridhisha ikizingatiwa wachezaji wengi katika timu yake ni wapya.
”Watu wengi wamezoea mimi huwa nachapwa, napetoza mechi kiholela ila hilo limeacha. Ukiangalia mechi zetu za hivi punde zaidi nimekuwa nikirekebisha makosa madogo madogo na ukiangalia kikosi kinazidi kuimarika. Kwa sasa naeza sema Inter Dabaso ajipange manake mechi ijayo nakutana naye na yeye mwenyewe ataona.”

