Mataifa 21 yalianza rasmi kuwasili mjini Mombasa jana tayari kwa kushiriki katika mashindano ya makala ya 11 ya Tong Ill Moo doo Opens ambayo yanaanza rasmi hii leo katika ukumbi wa akademia ya Agha Khan.
Hata hivyo katika taarifa za awali ni kuwa mashindano hayo yamevutia takriban mataifa 42 kutoka pande mbalimbali za dunia.
Timu ya Kenya ikiongozwa na rais wa shirikisho la mchezo huo Clarence Mwakio imethibitiosha kuwa inalenga kutetea ubingwa wake wa 11.
Kulingana na Mwakio kucheza katika ardhi ya nyumbani pamoja na kushirikisha wachezaji wengi wa kike na kiume katika mchezo huo ndio siri kubwa inayowapa motisha wa kuandikisha matokeo mazuri.
”Siku zote mcheza kwao hutuzwa na siri kubwa ya mafanikio yetu ni kujituma zaidi tunapokuwa katika ardhi ya nyumbani. Pia tumekuwa tukishirikisha wachezaji wengi katika kikosi chetu jambo ambalo limetusaidia sana kushinda matuzo mengi. Sio hapa ndani tu lakini pia nje. Alafu Mombasa imekubalika kimataifa kuwa inauwezo wa kuandaa mashindano kama haya na ndio maana mataifa mengi kipindi hiki yatakuwepo hapa kuchuana nasi. Tunaimani tutatetea ubingwa.”

