Mkufunzi wa klabu ya Manchester United Eric Ten Hag amesema kuwa vijana wake jana walionyesha mchezo mzuri na hawakustahili kupoteza mechi yao dhidi ya Bayern Munich katika uwanja wa Old Trafford.
Ten Hag ambaye kikosi chake kimetolewa kabisa katika mashindano ya Uefa anasema katika kila idara klabu hiyo ilikuwa imara lakini matokeo ya kupigwa bao 1-0 haikustahili.
Ni mechi ambayo klabu ya United ilifanya mashambulizi matano pekee na kupiga shuti moja hatari jambo ambalo linakashifiwa na mashabiki wengi wa soka hasa kauli ya Eric Ten Hag ya kuwa walikuwa vizuri.
”Tulikuwa vizuri katika kila idara, mwanzo mwisho wa mechi tulionyesha ukakamavu lakini matokeo yalitukataa. Ndio tulipoteza lakini kwa kweli tulikuwa timu bora uwanjani. Nawaheshimu sana Bayern Munich ni timu nzuri lakini jana tulikuwa bora zaidi.” Alisema Ten Hag.
The Red Devils ndio wa mwisho katika kundi lao licha ya mwanzo wa msimu droo ilipotoka kuonekana kuwa wangekuwa kati ya timu ambazo zingeendelea.

