SIASA MICHEZONI ZAKASHIFIWA MAGARINI

Harrison Fondo ambaye ni mwenyekiti wa zamani katika shirikisho la soka tawi la eneo bunge la Magarini amekashifu vikali hulka ya viongozi kutumia vijana michezoni kujinufaisha au kupata umaarufu wa kisiasa baadala yake  kukuza michezo ili kusaidia vijana.

Amesema kwamba jambo hilo limeathiri soka la mashinani kwani vijana wamekuwa wakitelekezwa pindi tu baada ya uchaguzi kumalizika.

Katika mahojiano na Paps Mkare ambaye ni mwandishi wa michezo katika kituo cha Lulu Fm Fondo amenukulika akisema, ”Ninalaani vikali tabia ya baadhi ya viongozi mashinani kutumia vibaya michezo na vijana kwa kunufaisha wanasiasa kipindi cha uchaguzi na baadaye kuwatelekeza. Ni jukumu la viongozi waliochaguliwa kusaidia makuzi ya michezo baadala ya kujinufaisha kisiasa.”

Fondo ambaye sasa ni kiongozi wa vijana katika kanisa la Baptist eneo bunge la Magarini amesema kwamba kanisa hilo kwa ushirikiano na wainjilisti wa KuzaApp wanalenga kuanzisha mashindano ya michezo mbalimbali kipindi hiki cha likizo ili kuwahubiria vijana pamoja na kukuza Talanta.