Gavana wa zamani wa kaunti ya Nairobi ambaye amekuwa mdhamini wa matibabu ya bondia mkongwe Conjestina Achieng amethibitisha kwamba bondia huyo amerejea hali yake ya sawa baada ya kipindi kirefu cha masaibu ya kiafya alipokuwa katika kaunti ya Siaya.
Baada ya pigano la kirafiki dhidi ya bondia wenza Fatuma Zarika wikendi ilopita katika kaunti ya Mombasa Sonko anasema kwamba lengo lake sasa ni kuhakikisha maisha ya Congestina yanazidi kuimarika hata zaidi baada ya safari ndefu ya ukarabati wa afya ya mchezaji huyo.
”Saa hii Conjestina yuko sawa. Tumejaribu vile tunaweza kumtoa huko kwa mambo yake yaliyokuwa yanamsumbua akiwa Siaya. Saa hii ameanza mazoezi mdogo mdogo ili kuzidi kuwa sawa” Alisema Mike Sonko.
Wakati hayo yakijiri, Bondia wa Kenya Fatuma Zarika anajitarajisha kushuka ulingoni mwezi ujao katika kaunti ya Nairobi kwa pigano lake la kwanza baada ya muda.
”Najitayarisha kwa mashindano ambayo yatafanyika mwezi Julai jijini Nairobi. Mimi saa hii najitayarisha kwa mashindano hayo tu” Alisema Zarika.
Kwa sasa mpinzani wa bondia huyo bado hajabainika lakini Zarika anasema kwamba ako na imani atachukua ubingwa kutokana na anavyojiandaa.
”Serikali inafaa isaidie mavijanaa katika michezo hasa pia hii ya ndondi angalau mavijana wengi wajitokeze wacheze. Kingine ni kwamba wachezaji wanapitia changamoto nyinyi ambazo zinawafanya kutokuwa active katika michezo. Serikali inafaa kuweka fights nyingi ili wachezaji wengi waupende huu mchezo na wahisi kulipwa.” Aliongeza Zarika.
Zarika ametoa wito kwa serikali ya Kenya kuupiga jeki mchezo wa ndondi kwa kusaidia wachezaji kukuza vipaji vyao pamoja na kuhamasisha umma kuhusu mchezo huo ili kuufanya kuwa mchezo pendwa kwa wananchi wengi wa Kenya tofauti na hali ilivyo kwa sasa.

