WANAFUNZI 600 WADI YA GONGONI WANUFAIKA NA FEDHA ZA UFADHILI WA MASOMO

Jumla ya wanafunzi 600 katika wadi ya Gongoni eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi wamenufaika na kima cha shilingi milioni 4.8, fedha za ufadhili wa masomo kutoka kwa hazina ya ufadhili wa masomo ya wanafunzi wa kaunti ya Kilifi.
Kulingana na mwenyekiti wa kamati ya ugavi wa basari katika wadi hiyo David Mwanyule, idadi hiyo ni zaidi ya asilimia hamsini ya wanafunzi waliotuma maombi ya kupata fedha hizo.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mwanyule amesema wale waliokosa kupata basari hizo katika awamu ya kwanza ya zoezi hilo, watapewa kipaumbele katika awamu ya pili ya ugavi wa fedha hizo.
Kwa upande wake mwakilishi wadi ya Gongoni, Stephen Baya amesema kuwa hatua ya serikali ya kaunti ya kilifi kuongeza mgao wa fedha katika hazina ya ufadhili wa masomo ni kuhakikisha kuwa wazazi wanapigwa jeki katika kutekeleza jukumu lao la kuwasomesha wanao.