IDADI KUBWA YA WASICHANA WALIOFANYA MTIHANI WA KCPE KATIKA SHULE YA MSINGI YA BOFU WAKOSA KUJIUNGA NA SHULE ZA UPILI

Idadi kubwa ya wasichana waliofanya vyema katika mtihani wa KCPE kwenye shule ya msingi ya Bofu eneo bunge la Kilifi Kaskazini kaunti ya Kilifi, wamekosa kujiunga na shule za upili kutokana na kile ambacho kinadaiwa kuchangiwa na ukosefu wa karo.
Haya ni kwa mujibu wa katibu mkuu wa vuguvugu la vijana la KILIFI YOUTH ON THE MOVE kaunti ya Kilifi, Heri Kombe ambaye amesema kutokana na hali hiyo, sasa baadhi ya wasichana wamelazimika kuoleka katika eneo hilo.
Akizungumza mwanahabari wetu wakati wa kuendeleza zoezi la ugavi wa sodo kwa wasichana wa shule hiyo, katibu huyo ametoa wito kwa serikali na mashirika ya kijamii kujitokeza na kutoa misaada ya bidhaa hizo na hata ufadhili wa masomo kwa wanafunzi hao wa kike.
Kombe ametaja suala la umasikini kuwa mojawapo ya masuala ambayo, yamechangia pakubwa kudorora kwa elimu ya mtoto wa kike katika eneo hilo na kaunti ya KIlifi kwa jumla, kwa kile alichosema wazazi wengi huwaoza watoto wao wakiwa na umri mdogo ili kupata mahari, ambayo itawasaidia kukimu mahitaji ya familia.