KIPCHUMBA MURKOMEN ASEMA KUFIKIA MWISHONI MWA MWEZI APRILI KUTAKUWA NA MKURUGENZI MPYA WA KPA

Waziri wa uchukuzi na miundo mbinu nchini Kipchumba Murkomen amesema kufikia mwishoni mwa mwezi April mwaka huu wa 2023, Mamlaka ya bandari nchini KPA inatarajiwa kuwa na mkurugenzi mkuu mpya.

Akizungumza katika kaunti ya Mombasa Murkomen amesema Bodi ya KPA ndiyo ambayo ina jukumu la kumteua mkurugenzi mkuu ambaye atachukua nafasi ya John Mwangemi ambaye anatarajiwa kustaafu mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu wa 2023.

Murkomen ameitaka bodi hiyo kuendeleza mchakati huo ambao ulianzishwa na bodi ya zamani ya KPA.

Murkomen ambaye alikuwa amekutana na wanachama wapya wa bodi ya KPA ameitaka bodi hiyo kuhakikisha mchakato huo unatekelezwa kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mamlaka ya KPA Benjamin Tayari ameahidi wanachama wa bodi hiyo watashirikiana ili kumpata anayefaa kuwa mkurugenzi mkuu huku katibu mkuu katika wizara hiyo ya uchukuzi Nixon Korir akimpongeza John Mwangemi kwa utendakazi wake.