UKOSEFU WA USALAMA WATISHIA SOKA LAMU

Mkufunzi mkuu wa klabu ya Omax kutoka kaunti ya Mombasa, Juma Kalato ametoa wito kwa serikali ya kaunti ya Lamu pamoja na serikali kuu kuimarisha usalama katika kaunti hiyo.

Hofu ya mashambulizi kutoka kwa wanamgambo wa Alshabab ndio jambo ambalo linatishia vilabu ambavyo husafiri kucheza mechi za ugenini katika kaunti ya Lamu mbali na tatizo la ukosefu wa viwanja vyenye hadhi kwa sasa.

Kwa sasa kuna ugumu wa usafiri kwa kuenda Lamu ikizingariwa kwamba viwanja muhimu vya kuchezea mechi kubwa vinapatikana visiwani.

Mkufunzi Kalato aidha  ameshauri uongozi wa kaunti ya Lamu kujenga viwanja bora nje ya visiwa vya kaunti hiyo ili kurahisisha usafiri kwa wachezaji ambao kwa sasa husafiri kucheza na vilabu vinavyoshiriki ligi kubwa kama vile Deep Sea.