HUDUMA ZA MATIBABU ZATARAJIWA KUIMARIKA KAUNTI YA TAITA TAVETA

Mikakati mbalimbali inapoendelea kuwekwa na serikali ya kaunti ya Taita Taveta ili kuimarisha maisha ya wenyeji hasa kwenye idara ya afya, tayari mawaziri 6 wa kaunti hiyo wamekabidhiwa ofisi rasmi.
Miongoni mwao ni waziri wa afya Gifton Mkaya ambaye amekabidhiwa ofisi hiyo na aliyekuwa waziri wa afya John Mwakima, wakazi wakiwa na matarajio mengi kwa viongozi hao pamoja na gavana wa Taita Taveta Andrew Mwadime katika kuimarisha huduma za afya.
Akizungumza katika hospitali ya Rufaa ya Moi mjini Voi, waziri anayeondoka John Mwakima amesema wamemkabidhi waziri anayeingia mamlakani stakabadhi muhimu ambazo zitamsaidia katika kuimarisha sekta ya afya.
Kwa upande wake waziri wa afya kwenye kaunti hiyo Gifton Mkaya amesema atashirikiana na KEMSA ili kuhakikisha kuna madawa ya kutosha pamoja na vifaa vya matibabu ili huduma za matibabu ziboreke hata zaidi.