Klabu ya kaunti ya Kilifi Moving The Goalpost United imepata pigo baada ya shirikisho la soka nchini FKF kubatilisha msimu wa 2021/2022 na kusema kwamba hakuna klabu itapanda ama kushuka daraja.
MTG United ilikuwa imepanda daraja baada ya kuinyuka Gideon Starlets FC kwenye uwanja wa Nakuru mwezi Julai 24, 2022. Pande zote mbili zilimaliza kwenye nafasi ya pili kwenye zone A na B mtawalia hivyo kulazimika kumenyana ili kupata atakayefuzu kuingia ligi kuu ya wanawake nchini.
Ndoto ya MTG United ya kurudi Kenya Women Premier League sasa inasalia ngumu huku mkufunzi wa klabu hiyo Fathime Tibu akisema kwamba wanafanya kikao na uongozi wa klabu hiyo na watatoa tamko rasmi hivi punde.
“Ndio, tumeona taarifa za shirikisho na kwa sasa tunafanya kikao kupata the way forward. Tutajuza umma hivi punde tamko letu kufuatia uamuzi huo wa shirikisho,”Tibu alisema kupitia njia ya simu.
Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) lilitangaza Jumatano kuwa msimu wa Ligi Kuu ya FKF msimu wa 2021-2022 umebatilishwa.
Kamati ya Utendaji ya Kitaifa ya FKF ilisema baada ya mkutano wao kwamba ligi zote zilizochezwa msimu uliopita hazitatambuliwa na kwamba hakutakuwa na kupanda au kushuka daraja katika Ligi Kuu ya FKF, National Super League, na Ligi Kuu ya Wanawake.
“Ligi Kuu ya FKF ya 2021-2022, National Super League, Ligi Kuu ya Wanawake, Ligi Daraja la Kwanza kwa Wanaume, na Ligi ya Daraja la Kwanza ya Wanawake haitatambuliwa na imetangazwa kuwa batili.
“Aidha, hakutakuwa na kupandishwa daraja au kushushwa daraja katika Ligi Kuu ya FKF, Ligi ya Taifa ya Super League, na Ligi Kuu ya Wanawake,” ilisoma barua iliyotiwa saini na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa FKF Barry Otieno.
NEC pia ilisema kuwa ligi za FKF za Daraja la Kwanza kwa Wanaume na za FKF za Wanawake za Daraja la Kwanza hazitapanda daraja wala kushuka daraja.
“Uamuzi huo wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya FKF limeongozwa na Sheria za FKF, sheria za FIFA, Sheria na Kanuni za FKF (2019), na Mzozo wa Michezo,” alisema Otieno.
Hata hivyo NEC iliamua kuwa ligi za FKF za 2021/2022 za Ligi Daraja la Pili, Mikoa na Kaunti kuendeshwa na Matawi ya FKF, kwa mujibu wa sheria za FKF na FKF.

