EDISON CAVANI NA LUIS SUAREZ KUCHEZA KWA MARA YA MWISHO KOMBE LA DUNIA

Zimesalia siku 11 kabla ya mashindano ya kombe la dunia kuanza rasmi nchini Qatar na sawa na nyota wa Argentina Leonel Messi pamoja na Cristiano Ronaldo wa Ureno kucheza mashindano yao ya mwisho kwenye kombe la dunia mwaka huu, straika wa Uriguay Luiz Suarez pamoja na mwezake Edison Cavani msimu huu watakuwa wanacheza kipute hicho kwa mara ya mwisho.

Hii ni kulingana na kauli zao wenyewe awali ambapo wamehoji kuwa umri ndio kigezo kikuu kinachowafanya kustafu soka la kitaifa kwani sasa nguli hao wamefikisha miaka 35 kumaanisha wakati wa mashindano yajayo watakuwa na miaka 39.

Kwa zaidi ya muongo mmoja nyota hao wamewakilisha Uruguay katika mashindano ya kimataifa ambapo Suarez amefunga mabao 68 ndani ya mechi 134 wakati Edison Cavani akifunga mabao 58 katika mechi 133.

Waliisaidia timu yao kufika hatua ya robo fainali katika mashindano ya kombe la dunia la mwaka 2010 kabla ya kushindia taifa lao kombe la Copa Amerika mwaka 2011.