Msimu mpya wa ligi kuu ya FKF nchini Kenya wa mwaka 2022/2023 huenda ukaanza kati ya tarehe 12-20 mwezi November mwaka huu. Hii ni kulingana na wakufunzi wakuu wa vilabu vinavyoshiriki ligi ya Kenya Premier League baada ya kikao na mkurugenzi mkuu wa fkf Barry Otieno hapo jana.
Haya yanajiri baada ya muda wa kamati ya mpito ilopewa jukumu la kusimamia soka nchini kutamatika rasmi wiki jana.
Kwa sasa bado vilabu vya ligi kuu ya fkf pamoja na shirikisho la soka wanaendelea na mazungumzo kulainisha hali ya soka nchini kabla ya kuhusisha fifa kwa lengo la kuondoa taifa hili kwenye marufuku ya kutoshiriki mechi za kimataifa.
Kenya iliadhibiwa na FIFA marufuku hiyo kutokana na serikali kuingilia masuala ya FKF pale ambapo waziri wa michezo wakati huo balozi Amina Mohamed alibandua shirikisho la soka kutokana na madai ya ubadirifu wa fedha na matumizi mabaya ya kiofisi.

