MASENETA KANDA YA PWANI WAPONGEZWA

Mshirikishi wa masuala ya kijamii katika eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi Ahmed Mahmood almaarufu Akuku, amewapongeza maseneta wa eneo la Pwani katika bunge la seneti, kwa kumpigia kura aliyekuwa gavana wa kaunti hii Amason Kingi ili kuwa spika wa bunge hilo.

Kwa mujibu wa Ahmed viongozi hao walionyesha mfano bora kwa wanajamii katika ukanda huu, kwani hawakufanya uamuzi kulingana na misimamo yao ya kisiasa ama mirengo.

Akizungumza katika wadi ya Gongoni, amesema kuwa hatua ya maseneta wa Pwani kutilia maanani mila na desturi za eneo hili, ndiyo chanzo cha wao kuweka kando tofauti zao za kisiasa katika kipute cha kuwania uspika wa seneti.

Aidha Ahmed  amemtaka gavana wa kaunti hii Gideon Maitha Mung’aro, pamoja na naibu wake Flora Chibule kutowatupa nje baadhi ya viongozi waaminifu, ambao pia walikuwa mawaziri katika serikali ya aliyekuwa gavana wa kaunti hii Amason Kingi, kutokana na hatua ya wao kukosa kumuunga mkono katika kampeni zake.