Mwenyekiti wa kundi la kutetea haki za wananwake na Watoto la Kilifi Mums kaunti ya Kilifi Kibibi Ali amesema anaunga mkono kauli ya waziri wa elimu nchini Prof. George Magoha ya adhabu ya kiboko kurejeshwa shuleni.
Kibibi ambaye alikuwa akizungumza na mwanahabari wetu kwa njia ya simu amesema hatua hiyo itasaidia kudhibiti visa vya watoto kupotoka kimaadili.
Amesema tangu kuondolewa kwa adhabu hiyo shuleni watoto wengi wamepotoka kimaadili ikilinganishwa na miaka ya nyuma wakati ambapo wanafunzi walikuwa wakiadhibiwa shuleni.
Kwa mujibu wa Kibibi wamekuwa wakipokea kesi nyingi za utovu wa nidhamu kutoka kwa watoto wengi na kusema ni lazima hatua thabiti zichukuliwe ili kudhibiti visa hivyo.
Aidha, amewataka walimu kutowaadhibu watoto shuleni kutokana na hasira zao ili kutowajeruhi wanafunzi na kuwataka kutopitiliza adhabu kwa wanafunzi.
Kibibi amewataka wazazi wa kiume na kike kushirikiana katika kuwalea watoto wao kwenye misingi inayofaa ili wasipotoke kimaadili.
KIBIBI ALI AUNGA MKONO KAULI YA MAGOHA YA KUTAKA ADHABU YA KIBOKO IREJESHWE SHULENI

