Muungano wa raga nchini Kenya umefanya uchaguzi wa viongozi wapya usiku wa kuamkia leo na Ian Mugambi amechaguliwa kama katibu mkuu wa muungano huo aliposhinda kura 18 mbele ya mpinzani wake wa karibu Raymond Olendo aliyepata kura 13.
Moses Ndale ameibuka mshindi wa wadhifa wa naibu mwenye kiti kwa kupata kura 20 mbele ya Peris Mutoko aliyepata kura 11
Oscar Mango amepata kura 23 za kumwezesha kushinda wadhifa wa mkurugenzi mkuu pamoja na Leslie Mwangale na kuwaangusha Hillary Itela na Charles Chege waliomaliza katika nafasi ya tatu na nne mtawalia.
Mweka hazina Joshua Aroni amefanikiwa kuhifadhi wadhifa wake bila kupingwa. Mwenyekiti wa muungano huo Oduor Gangla akizungumza baada ya uchaguzi huo amesema kuwa kwa sasa wanalenga kuanza vikao vya kufanya marekebisho ya katiba.
Kikosi cha raga cha Kenya cha wachezaji saba kila upande sasa kinalenga kuingia kwenye mashindano ya kombe la dunia kwa mara ya sita. Macho yote ya wakenya wapenda raga yatakuwa yanaelekea Afrika Kusini ambapo kikosi hicho kinachofunzwa na mkufunzi Damian McGrath kitakuwa kinarindimana kwenye mashindano yanayotarariwa kuanza rasmi wikendi hii.
Ikumbukwe kuwa Kenya imeshiriki katika mashindano yote ya kombe la dunia kuanzia mwaka 2001 mpaka leo na sasa mpinzani wao mkuu katika bara hili la Afrika anasalia kuwa Afrika Kusini.

