ZAIDI YA VIJANA ELFU NNE KAUNTI YA KWALE WADAIWA KUWA KATIKA HATARI YA KUPATA VIRUSI VYA UKIMWI.

Zaidi ya vijana 4,000 wanaotumia dawa za kulevya katika kaunti ya Kwale, wako kwenye hatari ya kuambukizwa na hata kueneza maambukizi ya virusi ya Ukimwi.

Haya ni kutokana na kusitishwa kwa ufadhili wa mipango ya kupunguza maambukizi hayo na shirika la misaada la Marekani – USAID na hazina ya Global Fund, ambayo imewasaidia kupata sindano mpya za kujidunga, ili kuepuka maambukizi ya HIV.

Akizungumza na waandishi wa habari kaunti hiyo, mkurugenzi wa shirika la kijamii la Teenswatch, Cosmus Maina amesema idadi kubwa ya miradi ya shirika hilo sasa, imelemazwa kutokana na ukosefu wa fedha za kuiendesha.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya afya katika bunge la kaunti ya Kwale, Mwagawari Mwanyae ametoa wito kwa wadau wa afya na serikali ya kitaifa, kushirikiana ili kuhakikisha mipango ya kutoa sindano na dawa za methadon haififii.