GAVANA WA KAUNTI YA KIAMBU APINGA MADAI YA KUSHIRIKI UFISADI.

Gavana wa kaunti ya Kiambu, Kimani Wamatangi amesema kuwa hatua yake kukamatwa na maafisa wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC ni njama ya kumhangaisha na kujumu siasa zake.

Kulingana na gavana huyo, alipokea simu kutoka na mmoja wa wanasiasa wakuu katika taifa hili, ambaye aliahidi kumhangaisha iwapo hatakubaliana na matakwa yake.

Akizungumza baada ya kuachiliwa na maafisa hao wa DCI katika kaunti ya Nairobi, Wamatangi amesema kuwa kamwe hatakubali kutishiwa na wanasiasa wengine kutokana na utendakazi wake katika serikali ya kaunti hiyo na kitaifa.

Vile vile gavana Kimani, ameibua madai ya biashara yake kuvamiwa na wahuni pale jijini Nairobi, anaodai walitumwa na mahasidi wake wa kisiasa na tayari ameandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Lang’ata.

Aidha, Jumla ya shilingi milioni 12 na dola elfu 13 za Marekani zilipatikana katika maakazi ya gavana huyo, kwenye oparesheni iliyoendelezwa na maafisa wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC.

Maafisa hao walivamia makaazi ya gavana huyo siku ya Jumanne tarehe 15 mwezi machi mwaka 2025 asubuhi, ili  kubainisha madai ya ufujaji wa fedha katika mkataba wa udanganyifu yenye thamani ya shilingi bilioni 1.5.

Wamatangi alikamatwa pamoja na maafisa wengine wa serikali ya kaunti ya Kiambu.