Huenda wikendi ijayo klabu ya Young Bulls isisafiri kushiriki mechi yake ya ligi ya fkf katika daraja la kwanza kitaifa dhidi ya klabu ya Kabati Youth. Hii ni kutokana na tukio la wachezaji wote kuambiwa wafunge firago na kuondoka katika kambi ya klabu hiyo kwa kile kilichotajwa kuwa likizo ya lazima.
Bila shaka taarifa hii imethibitishwa na kocha wa klabu hiyo Ali Mwachaunga, Aliyekuwa nahodha wa klabu hiyo Shauri Mulewa pamoja na meneja mpya Hussein Captain Garga.
Kulingana na taarifa za kuaminika ni kuwa huenda wakarejea Jumatatu wiki ijayo baada ya mmiliki wa klabu hiyo Mhandisi Johnson Mwabati atakapokuwa amepiana mwongozo mpya, Kwa sasa taarifa zinasema kuwa wachezaji wote pamoja na benchi la kiufundi wako nyumbani wakisubiri maamuzi ya mwenye timu.
Taarifa zaidi zinasema kuwa Mwabati alitimua timu nzima wikendi ilopita baada ya kipigo cha sita msimu huu walipopoteza nyumbani dhidi ya klabu ya Congo Boys katika uwanja wa Alaskan.
Young Bulls imekuwa na msururu wa matokeo duni msimu huu ikisimama katika nafasi ya mwisho katika jedwali wakiwa na alama nne baada ya ushindi mmoja na sare moja katika mechi nane.

