Waziri wa Leba Dkt. Alfred Mutua amepinga madai kwamba serikali iliwapora na kuwalaghai wakenya kwenye mpango wa kazi majuu wa kuwatafutia kazi Ughaibuni.
Kulingana na waziri Mutua, zaidi ya wakenya elfu 41 wamenufaika kupata nafasi hizo za ajira ughaibuni na kuongeza kuwa mtu anaweza pata kazi hizo kwa kati ya mwezi mmoja hadi kumi na miwili na hivyo kuwataka wakenya hao kuwa na subra.
Akizungumza mbele ya kamati ya leba katika bunge la seneti, Waziri Mutua amesema kuwa serikali haikuwalaghai wakenya, katika suala hilo na hivyo wanapaswa kuendelea kusubiri kwani baadhi ya waajiri huchukua mda kuidhinisha stakabadhi za wale wanao tuma maombi ya kupata kazi hizo.
Ni kauli ambayo imegadhabisha pakubwa maseneta katika kamati hiyo wakiongozwa na seneta mteule Gloria Orwoba huku wakimtaka waziri huyo kufafanua suala la uhalali wa kampuni zilizotumika katika zoezi la wakenya kutuma maombi ya kupata nafasi za ajira ughaibuni.