Naibu kinara wa Chama Cha ODM ambaye pia ni gavana wa Kaunti ya Mombasa Abdulswamaad Shariff Nassir, amepinga vikali mapendekezo ya aliyekuwa kinara wa Chama hicho Raila Odinga, kutaka kuondolewa kwa hazina ya maendeleo ya maeneo bunge nchini CDF.
Akizungumza katika gatuzi dogo la Jomvu, Nassir amesema hatua hiyo itapunguza juhudi za maendeleo nchini huku akisisitiza ushirikiano kati ya wabunge na serikali za Kaunti, kwa minajili ya maendeleo katika Kaunti wanazoziongoza.
Nassir ameongeza kuwa Kuna mikakati ya kuwawezesha wawakilishi wadi pia, kuwa na hazina itakayosaidia kutekeleza shughuli mbalimbali katika kiwango Cha wadi.
Nassir vilevile ameshikilia msimamo wake wa kutaka Fedha za usimamizi wa ujenzi wa barabara mbalimbali katika Kaunti zao kusimamiwa na serikali hizo badala ya serikali kuu.