WENYEJI WA SAKA WANAHOFIA KUENDELEA KUVAMIWA NA VIBOKO

Wenyeji wa eneo la Saka kaunti ya Tana River wanahofia kuendelea kuvamiwa na viboko baada ya kijana mwenye umri wa miaka 16 kushambuliwa na kiboko na kuaga dunia.
Marehemu Mohammed Abdi anadaiwa kushambuliwa na kiboko alipokuwa anachunga mifugo karibu na mto Tana.
Akithibitisha kisa hicho chifu wa eneo hilo Mumina Harun amesema viboko wamekuwa wakitoka ndani ya Mto Tana na kuingia kwenye vichaka vilivyoko karibu na makazi ya watu wakitafuta malisho.
Kwa upande wa wenyeji wa eneo hilo wanadai hali ya ukame kwenye kaunti hiyo ndicho chanzo cha viboko hao kuvamia wenyeji na wameitaka KWS kuweka mikakati ya kuwadhibiti ili kupunguza visa vya watu kuaga dunia.
Wanasema iwapo mikakati haitawekwa ya kuwadhibiti viboko hao huenda visa hivyo vikaongezeka hata zaidi.