MFUMO WA ELIMU WA CBC WAZIDI KUIBUA HISIA MSETO MIONGONI MWA WENYEJI WA KILIFI

Baadhi ya wazazi kaunti ya Kilifi wanasema wangali wanaunga mkono mfumo wa elimu wa umilisi CBC na kuitaka serikali kuu kuundeleza licha ya changamoto mbalimbali kushuhudiwa katika kuufanikisha.
Wazazi hao wakiongozwa na George Tune na Joseph Punga wamesema masomo ambayo yanafunzwa wanafunzi shuleni yanawawezesha kuwa na ujuzi zaidi ambao wanasema unawafaa hasa katika karne hii ya 21 ambayo teknolojia inazidi kubadilisha mambo mengi.
Wametoa wito kwa wazazi kuuthamini mfumo huo wa elimu licha ya kuwa unawafanya kugharamika zaidi kifedha.
Ni kauli ambayo imeungwa mkono na mwenyekiti wa shirika la kutetea haki za wanawake na watoto la KILIFI MUMS kaunti ya Kilifi Kibibi Ali ambaye ameusifia mfumo huo wa elimu akisema unasaidia kwa kiwango kikubwa kukuza talanta na vipaji vya wanafunzi shuleni na kutoa wito kwa serikali kutenga fedha zaidi katika sekta ya elimu ili kuwapunguzia wazazi gharama.