WAZIRI MUTURI AKABILIWA NA TISHIO LA KUBANDULIWA MAMLAKANI NA VIONGOZI WA BUNGE LA KITAIFA.

Baadhi ya wandani wa rais Willima Ruto sasa wanatishia kuwasilisha hoja ya kumbandua waziri wa Utumishi wa Umma Justine Muturi mamlakani kutokana na hatua yake kukashifu suala la utekajinyara linalo endelezwa na maafisa wa polisi nchini.

Wakiongozwa na mbunge wa Mugirango Kusini kaunti ya Kisii Silvanus Osoro amesema kuwa waziri Muturi hakupaswa kutoa kauli kuhusiana na masuala ya serikali kuendeleza visa vya utekajinyara kwani ni mmoja wa viongozi wanaotumikia serikali ya Kenya kwanza.

Osoro amemtaka waziri Muturi kujitokeza na kukanusha semi ambazo alitoa kwenye kikao na waandishi wa habari la sivyo viongozi wa bunge la kitaifa watapitisha hoja ya kumuondoa mamlakani pindi watakapo rejea bungeni baada ya siku 13.

Kwa upande wake waziri Justine Bedan Njoka Muturi amesema kuwa kamwe hatotishwa na suala la kubanduliwa mamlakani kwani anafahamu hakika kile alichozungumza kuwa ni kweli.

Waziri Njoka ameongeza kuwa alipofanya uamuzi wa kukubaliana na uteuzi wake kwenye baraza la mawaziri nchini alifahamu hakika katiba ya taifa hili kuhusiana na masuala ya kubanduliwa mamlakani.