WASHUKIWA WA MAUAJI YA AFISA WA IEBC KAUNTI YA KILIFI AISHA ABUBAKAR WAFIKISHWA KATIKA MAHAKAMA YA SHANZU.

Mahakama ya Shanzu imeamuru kuzuiliwa kwa siku 21 kwa washukiwa wawili wanaohusishwa na mauaji ya marehemu afisa mkuu wa IEBC kaunti ya Kilifi Aisha Abubakar.

Washukiwa hao wawili, Joseph Sunday na Brian Templer Oyere, wanadaiwa kuhusika katika mauaji ya kikatili ya Aisha, yaliyofanyika nyumbani kwake eneo la Utange, kaunti ya Mombasa.

Kulingana na hakimu mkuu wa mahakama ya Shanzu Leah Juma amewataka wawili hao kuendelea kuzuiliwa katika kituo cha Polisi cha Bamburi kaunti ya Mombasa.

Vile vile ameongeza kuwa washukiwa hao pia watafikishwa hospitalini ili kufanyiwa uchunguzi wa afya ya kiakili.

Aidha Hakimu Leah amekubaliana na ombi la kutowapatia washukiwa hao dhamana ili kuendeleza kesi hiyo wakiwa inje ya mahakama kwa kile alichosema kuwa kesi hiyo ina uzito mkubwa na inafuatiliwa sana na umma huku akitoa wito kwa mamlaka ya kuchunguza utendakazi wa polisi IPOA kuchunguza madai ya wahasiriwa kuhasiriwa na maafisa wa polisi.

Kesi hiyo imeratibiwa kusikilizwa tena mnamo tarehe 6 mwezi februari mwaka 2025.