WAPEMBA ELFU 7 KUSAJILIWA KUPATA VITAMBULISHO VYA KITAIFA

Zoezi la kuwasajili wapemba kama kabila la 47 nchini Kenya limeanza katika kaunti ya Kilifi.
Zaidi ya wapemba 7,000 wanatazamiwa kusajiliwa kupata vitambulisho katika kipindi cha mwezi mmoja.
Katibu wa uhamiaji na huduma za umma nchini Julius Bitok amesema zoezi hilo la Kuwasajili Wapemba litafanyika kwa mwezi mmoja katika kaunti za Mombasa, Kilifi na Kwale wanapoishi Wapemba.
Naye mbunge wa Kilifi Kaskazini kaunti ya Kilifi Owen Baya ametoa wito kwa katibu huyo kuanza pia usajili wa jamii wa Warundi ili wawe Wakenya halisi.
Kwa upande wake gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Maitha Mung’aro ameipongeza serikali kuu kwa kuitambua jamii akisema wamekuwa wakipitia wakati mgumu wanapohitaji msaada wowote huku Julius Bitok akiwasihi Wapemba kujitokeza kwa wingi ili kusajiliwa.
Ni zoezi ambalo linajiri miezi miwili baada ya rais William Samoei Ruto kuamuru Jamii hiyo kupewa uraia wa taifa hili la Kenya.