WANAWAKE MJINI MALINDI WAHIMIZWA KUFIKA KWENYE VITUO VYA AFYA KUJIFUNGUA

Wanawake eneo bunge la Malindi na kaunti ya Kilifi kwa jumla, wametakiwa kuhakikisha wanajifungua katika vituo vya afya, kama njia mojawapo ya kujilinda dhidi ya athari ambazo huenda zikawakumba wakati wanapojifungua majumbani.
Haya ni kwa mujibu wa afisa wa afya ya umma katika eneo la Malindi kaunti ya Kilifi, Thomas Kiboni ambaye amesema idadi kubwa ya wanawake wamekuwa wakivuja damu kupita kiasi wakati wanapojifungua majumbani kutokana na kutokuwepo kwa wakunga wa kuwasaidia.
Akizungumza katika hospitali kuu ya kaunti ndogo ya Malindi, afisa huyo wa afya amesema hatua hiyo pia imechangia kwa watoto wanaozaliwa kukumbwa na changamoto mbalimbali za kiafya, jambo ambalo huathiri afya zao wanapozaliwa.
Vilevile, Kiboni amewasihi akina mama kujisajili katika mpango wa linda mama, ulioanzishwa na serikali kuu kwenye utawala wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta kuhakikisha wanafika katika kliniki zilizoko karibu na makaazi ya ili kupata ushauri wa daktari kuhusiana na jinsi ya kulinda afya ya mtoto wao wakati mama anapokuwa mjawazito.